WAZIRI AKUTANA NA UJUMBE KUTOKA CHINA.-May 2019

Ujumbe wa Wizara ya Kilimo ya China umekutana na Uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili,Mifugo na Uvuvi wa Zanzibar kwa lengo la kushirikiana katika Uvuvi wa bahari kuu. Wakiwa ofisini kwake Maruhubi Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mhe Mmanga Mjengo Mjawiri alipata na nafasi ya kuzungumza na ujumbe huo wenye lengo la kujenga mashirikiano katika uvuvi wa bahari kuu sambamba na kuangalia aina mbalimbali za samaki ambao wanapatikana katika bahari hiyo ili kuweza kuedeleza shughuli za uvuvi hapa nchini kwa maslahi ya taifa . Mhe Mjawiri amefahamisha kua mashirikiano hayo katika sekta ya uvuvi yatawezesha wavuvi kuweza kupiga hatua ya kimaendeleo katika kuongeza ufanisi wa shughuli zao za uvuvi kwani Wizara pia imejipanga kuwawezesha wavuvi wadogo wadogo ili kuweza kufikia lengo walilokusudia. . Nae Naibu Katibu Mkuu aneshughulikia masula ya uvuvi Dkt Omar Ali Ameir amefahamisha kua Wizara ya Kilimo ya China tayari imeshandaa meli mbili ambazo zinategemewa kuja hapa kwa ajili ya majaribio katika bahari kuu na kuangalia raslimali nyengine inayoweza kupatikana mbali na aina ya samaki wa jodari ambao ndio huvuliwa katika bahari hiyo. Amefahamisha kua matokeo yatayopatikana katika majaribo hayo ndio yataweza kuleta fursa ya kuweza kuendeleza shughuli za uvuvi na kufikia lengo lililokusudiwa ndani ya sekta ya uvuvi sambamba na kuutaka ujumbe huo kuweza kuwasaidia katika ujenzi wa miundombinu ya bandari pemba. Ujumbe wa Wizara ya Kilimo ya China upo Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo ya Zanzibar kwa mazungumzo ya pamoja na makubaliano ambayo yatawezesha zanzibar kuweza kupiga hatua mbele katika sekta ya uvuvi hapa nchini na kuinua pato la taifa kwa maendeleo ya wananchi wake na taifa kwa ujumla.